"ACC haijamjibu Bi Siddiq"
Mamlaka ya kukabiliana na ufisadi nchini Bangladesh imetoa hati ya kukamatwa kwa mbunge wa chama cha Labour Tulip Siddiq kwa madai ya ulaghai wa ardhi.
Tume ya Kupambana na Ufisadi nchini (ACC) inadai kuwa Bi Siddiq alipokea shamba lenye ukubwa wa sq 7,200 huko Dhaka kwa njia zisizofaa.
Mawakili wa Bi Siddiq walikanusha madai hayo.
Walisema: “Madai hayo ni ya uongo kabisa na yameshughulikiwa kwa maandishi na mawakili wa Bi Siddiq.
"ACC haijamjibu Bi Siddiq au kuweka madai yoyote kwake moja kwa moja au kupitia mawakili wake.
"Bi Siddiq hajui lolote kuhusu kesi iliyosikilizwa huko Dhaka inayohusiana naye na hana ufahamu wa hati yoyote ya kukamatwa ambayo inasemekana kutolewa."
Mbunge huyo alijiuzulu kama waziri wa Hazina mapema 2025 baada ya uchunguzi wa mshauri wa maadili wa waziri mkuu kuhusu uhusiano wake na shangazi yake, Sheikh Hasina.
Bi Hasina, waziri mkuu wa zamani wa Bangladesh, alitimuliwa mamlakani mwaka 2024 na kutoroka nchini mwezi Agosti baada ya wiki kadhaa za maandamano.
Anashutumiwa kwa kuzidi kuwa mtu wa kiimla, na kukamatwa kwa sababu za kisiasa na ukiukwaji wa haki za binadamu chini ya serikali yake.
Bi Hasina anakanusha makosa yote na kuyataja kuwa ni uwindaji wa wachawi wa kisiasa.
Katika barua yake ya kujiuzulu, Tulip Siddiq alikanusha madai hayo lakini akasema kwamba kubaki katika jukumu lake kunaweza kuwa "kukengeusha kazi ya serikali".
Mawakili wa Tulip Siddiq walisema: “Ili kuwa wazi, hakuna msingi wowote wa mashtaka yoyote kufanywa dhidi yake, na hakuna ukweli kabisa katika madai yoyote kwamba alipokea kiwanja huko Dhaka kwa njia zisizo halali.
"Hajawahi kuwa na shamba nchini Bangladesh, na hajawahi kushawishi ugawaji wa mashamba kwa wanafamilia wake au mtu mwingine yeyote."
Hapo awali iliripotiwa kuwa kiongozi wa muda wa Bangladesh alidai kuwa Bi Siddiq alikuwa na "utajiri ulioachwa" nchini humo "na anapaswa kuwajibika".
Katika maoni yake ya kwanza tangu kuondoka serikalini, Bi Siddiq alisema:
"Kumekuwa na madai kwa miezi kadhaa na hakuna mtu aliyewasiliana nami."
Timu yake ya wanasheria hapo awali ilielezea mashtaka hayo kama "ya uwongo na ya kuudhi".
Waliongeza: "Hakuna ushahidi wowote ambao umetolewa na ACC kuunga mkono tuhuma hii au nyingine yoyote iliyotolewa dhidi ya Bi Siddiq, na ni wazi kwetu kwamba mashtaka hayo yanachochewa kisiasa."